Thursday, September 8, 2011

2nd Shear Charity Ball Opening ( Press Conference )
JARIDA la urembo na mitindo ya nywele la Shear (Shear Hair & Beauty Magazine) linaadhimisha miaka miwili ya kuwapo katika biashara kwa kuandaa tafrija ya hisani yenye lengo la kuchangisha fedha zitakazowezesha kufanyika kwa upasuaji wa bure kwa wanawake wanaosumbuliwa na maradhi ya fistula katika hospitali ya CCBRT sambamba na kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika hospitali ya Amana.

Tafrija hii ya hisani itafanyika Oktoba 1, 2011 kuanzia saa 1:00 usiku katika ukumKivukoni uliopo kwenye hoteli ya Movenpick Royal Palm.

Katika tafrija ya kwanza iliyofanyika mwaka jana katika hoteli ya Double Tree by Hilton, kiasi cha shilingi milioni 15 kilichangwa na nusu ya fedha hizo zikapelekwa CCBRT kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa fistula kwa wanawake waliokuwa na uhitaji wa tiba hiyo na kiasi kingine kikapelekwa katika Kijiji cha kulelea watoto cha SOS kilichopo Dar es Salaam ambako fedha hizo zilitumika kuchangia ada kwa watoto waliokuwa wakipata elimu katika kijiji hicho.


Kupitia tukio hili, tumeamua kutoa elimu kwa umma kuhusu maradhi haya yanayotibika ya fistula ambayo kwa karne nyingine yamekuwa na athari mbaya katika utu wa mwanamke. Ni jambo la kheri kwamba, hospitali ya CCBRT imekuwa ikitoa tiba ya bure kwa wanawake na hivyo kuwarejeshea utu ambao umekuwa ukitishiwa na maradhi haya.

Hospitali ya Amana kwa upande wake inakabiliwa na tatizo la maji inayosababishwa na uchakavu wa mabomba ya maji safi na maji taka, wenye uwezo mdogo wa kusafirisha majitaka hali inayoathiri ufanisi katika shughuli za usafi kwenye maeneo ya karibu na hospitali hiyo. Iwapo mfumo huo utaimarishwa, hospitali itaimarisha uwezo wake wa kutoa huduma bora na salama kwa wagonjwa na wafanyakazi na hivyo kudhibiti maambukizi kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Hospitali ya Amana inahudumia wastani wa wagonjwa 1,500 kwa siku na watoto wapatao 100 wanazaliwa hapo kila siku. Hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la kukosekana kwa vyanzo salama vya maji na mfumo duni wa majitaka, hali ambayo ni ya hatari kwa utendaji kazi wake. Hospitali inahitaji kisima kimoja cha maji kitakachojengewa pampu ya kusukuma maji na kuboreshwa kwa mfumo wake wa majitaka ili kuimarisha hali hii mbaya iliyopo sasa.

Tafrija hii ya hisani ya mwaka jana lilikuwa ni yenye mafanikio ya kutia moyo. Tunaamini jamii inaiunga mkono dhamira yetu hiyo njema na kuungana nasi tena katika tukio la Oktoba Mosi ili kusaidia kufikia malengo tuliyojiwekea.

Tunapenda kuzishukuru taasisi zifuatazo ambazo tayari zimeonyesha dhamira ya kweli ya kusaidia malengo haya muhimu; Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirikia la Nyumba la Taifa (NHC), Billicanas Group, Fly540, MaxCom, Precision Air, DeskTop Production (DTP), Hoteli ya Peacock, Clouds Radio na Clouds TV, Kampuni ya vifaa vya ujenzi SS Concrete, Benki ya Azania, BenchMark Production, Advertising Dar, Pepsi, Tanzania House of Talent (THT), I-View Media, mafuta ya kulainisha ngozi CocoTan, duka la nguo la Tina Maria, Kampuni ya kupamba masherehe ya Hugo Domingo, Imaging Smart na taasisi nyingi nyingine za Dar es Salaaam.

Tunapenda kuzitia moyo taasisi na watu wengine binafsi kujitokeza na kuchangia katika tafrija yetu hii ya hisani kwa kufika au kwa kuchangia ili kuifanya dunia iendelee kuwa sehemu nzuri na bora zaidi ya kuishi kwa wanawake wenye fistula ambao wanahitaji tiba na uangalizi wa CCBRT na wagonjwa kwa mamia wanaopata huduma katika hospitali ya Amana kila siku.

No comments:

Post a Comment